Diwani atupwa rumande kwa kuhamasisha fujo


MKUU wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, Kasika Majura ameamuru kuwekwa mahabusu kwa Diwani wa Kata ya Malinyi, Said Tilla kwa kukiuka agizo la Rais John Magufuli la kuzuia maandamano yasiyo na tija na badala yake kuhamasisha wananchi kufanya kazi.

Habari kutoka wilayani humo zinasema, diwani huyo anadaiwa kushawishi, kuhamasisha na kuandaa maandamano ya waendesha bodaboda wanaopinga kitendo cha askari polisi kuwakamata mara kwa mara kutokana na kukiuka sheria za barabarani kwa kuelekeza waandamanaji hao kwenda kwa DC juzi.

Akizungumzia tukio hilo, DC Majura alisema pamoja na diwani huyo kuwahamasisha madereva hao wa bodaboda kujitokeza kwa wingi ili kuandamana, pia hakuwaombea kibali jambo ambalo ni kosa kisheria, lakini pia alikiuka agizo la Rais la kuwataka wanasiasa kujiepusha na siasa badala yake wasimamie wananchi kuchapa kazi.

Mbali ya maandamano hayo kusababisha usumbufu kwa wananchi na kuvuruga utendaji wa kazi, pia yalivuruga ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe aliyokuwa aifanye wilayani Malinyi.

DC Majura alisema mbali ya kuandaa maandamano hayo, diwani huyo amekuwa mara kadhaa, akiwahamasisha wananchi katika kata yake kususa ushiriki wa shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Alitoa rai kwa wananchi wilayani hapo, kuepuka vitendo vinavyokiuka utaratibu wa sheria na uvunjifu wa amani kwa sababu hatakuwa na subira na mtu yeyote au kundi la watu litakalokiuka maagizo ya serikali.

Dk Kebwe aliagiza vijana wa bodaboda kupata mafunzo ya udereva katika Chuo cha Veta kilichopo wilayani humo na kuwahimiza kufuata sheria za barabarani pamoja na kushiriki ulinzi shirikishi kubaini wahalifu wanaoweza kutumia vyombo vyao vya usafiri kufanya uhalifu.
Previous
Next Post »