KESI ya kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh bilioni 5.4 inayomkabili Raia wa China, Yang Feng Glan maarufu kama “Malkia wa meno ya tembo” na wenzake inatarajiwa kuanza kusikilizwa Oktoba 5, mwaka huu.Hakimu Mkazi, Huruma Shahidi, alisema hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Awali, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Faraja Nchimbi alidai kuwa, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) amewasilisha kibali cha kuiruhusu Mahakama ya Kisutu kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi.
DPP ametoa kibali hicho kwa kuwa kisheria, Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi ambazo husikilizwa katika Mahakama Kuu.
Hakimu Shahidi aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 5, mwaka huu, kwa ajili ya kuwasomea washitakiwa maelezo ya awali pamoja na kuanza kusikiliza kesi hiyo.
Mbali na Glan, washitakiwa wengine, ni wafanyabiashara raia wa Tanzania Salivius Matembo (39) na Manase Philemon (39), wote wanashtakiwa kwa makosa manne.
Wanadaiwa kuendesha biashara ya nyara za serikali, vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 1,889 vya Sh trilioni 5.4, mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


ConversionConversion