Hospitali ya Taifa Muhimbili, inataraji kupeleka wataalamu saba nchini India Septemba 25, mwaka huu kwa ajili ya kujifunza upandikizaji wa kifaa cha usikivu (Cochlea Implant)Taarifa iliyotolewa na hospitali hiyo kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa hatua hiyo ni muendelezeo wa kutekeleza azma ya serikali ya kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ambao mara nyingi walikuwa wakifuata matibabu yasiyopatikana hapa nchini ama kutokana na kutokuwepo wataalam au ukosefu wa vifaa vya kutolea huduma husika.
"Katika kutekeleza hilo, Septemba 25, 2016, Hospitali ya Taifa Muhimbili itapeleka watalaam saba nchini India katika Hospitali ya Apollo iliyoko New Delhi ili wakajifunze kwa njia ya vitendo jinsi ya kufanya upasuaji na upandikizaji wa kifaa cha usikivu kwa watu wazima na watoto". Imeeza taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mtendaji wa hospitali hiyo, Prof Lawrence Museru.
Amesema kuwa wataalamu hao ni pamoja na madaktari bingwa wawili wa upasuaji wa pua, koo na masikio, wauguzi wawili wa chumba cha upasuaji, mtalaam mmoja wa kupima usikivu pamoja na wataalam wawili wa kufundisha jinsi ya kuongea hususani kwa watoto waliozaliwa na tatizo hilo.
Takwimu za Hospitali ya Taifa Muhimbili zinaonesha kuwa asilimia 95 ya wagonjwa ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji wa kuwekewa kifaa cha usikivu ni watoto wadogo hivyo hivyo mpango huo utasaidia watoto wengi hapa nchini na pia utajenga uwezo kwa wataalam wa ndani ya nchi.
Amesema gharama za kupandikiza kifaa cha usikivu kwa mtoto mmoja ni kati ya shilingi milioni 80 hadi 100 anapopelekwa nje ya nchi wakati mgonjwa mmoja anayepandikizwa figo nje ya nchi pia ikigharimu kiasi cha shilingi milioni 40 hadi 60.
Amesema uwepo wa huduma hizo hapa nchini utawezesha watanzania wengi kupata huduma hizo na kwa gharama nafuu zaidi na kupunguza mzigo kwa serikali wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwani gharama za matibabu zitapungua kwa zaidi ya asilimia 50.
Wataalam hawa wanatarajia kurejea hapa nchini Oktoba 28, 2016 tayari kuanza kutoa huduma hiyo.
Mapema mwezi huu Hospitali ya Taifa Muhimbili ilipeleka nchini India wataalamu 18 wa fani mbalimbali kwa ajili ya kujengewa uwezo wa upandikizaji figo kwa watu wenye matatizo ya figo ambapo timu hiyo inatarajia kurejea mwishoni mwaka huu.
"Gharama za kupeleka timu zote mbili ya upandikizaji wa figo pamoja na upandikizaji wa kifaa cha usikivu ni shilingi milioni 528 zikijumuisha gharama za mafunzo, nauli, fedha za kujikimu pamoja na gharama nyingine za mafunzo. Fedha hizi zote zitalipwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kujenga uwezo wa watalaamu wake". Amesema Prof Museru.


ConversionConversion