Dar es Salaam. Asilimia 96 ya wananchi wanakubali utendaji wa Rais John Magufuli ila wanaumizwa na ugumu wa maisha kwa sasa kiasi cha kuwa na hamu ya kumuuliza kuhusu mfumuko wa bei wa bidhaa na huduma, utafiti mpya wa Twaweza umebainisha.
Utafiti huo, uliozinduliwa jana jijini hapa, unaeleza kuwa kati ya matatizo yote ambayo wanakabiliana nayo, wananchi wangependa kumsikia Dk Magufuli akizungumzia suala la mfumuko wa bei.
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema katika utafiti huo, watu wawili kati ya 10 (asilimia 18) waliohojiwa walitamani kumuuliza Rais Magufuli atafanyaje kuhakikisha anapunguza ugumu wa maisha unaotokana na mfumuko wa bei.
“Hii ina maana kuwa wananchi wanataka kujua kutoka kwa Rais juu ya masuala ya fedha, mfuko wao utakuaje. Watu wanaguswa na thamani ya pesa yao,” alisema Eyakuze. “Hili ni jambo jipya kidogo kwa sababu masuala ya elimu na afya yamekuwepo katika kila utafiti kwa zaidi ya miaka mitatu ila hili kuhusu mfumuko wa bei na gharama za maisha ndiyo linaibuka sasa.”
Matokeo ya utafiti huo yanakuja wakati kukiwa na mjadala mzito juu ya ugumu wa maisha na kupungua kwa fedha katika mzunguko, jambo lililowafanya viongozi wa Serikali, akiwemo Gavana wa Benki Kuu (BOT), Profesa Benno Ndulu kueleza juzi kuwa hali ya uchumi ni shwari tofauti na inavyozungumzwa na viongozi wa kisiasa na wakosoaji wengine.
Licha ya wananchi kuonekana kuguswa na kupaa kwa gharama za maisha, takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kasi ya mfumuko wa bei imeendelea kupunguza hadi kufikia asilimia 4.9 mwezi Agosti kutoka asilimia 5.1 Julai, hicho kikiwa ni kiwango cha chini tangu Aprili mwaka jana.
Alipohojiwa kuhusu suala hilo, Profesa wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi alisema mara nyingi takwimu za mfumuko huwa ni wastani wa bei za bidhaa na huduma ambazo huenda zikagusa sehemu tu ya kundi la watu ndiyo maana wengine wanalalamika.
“Pamoja na mfumuko wa bei kushuka, bado wananchi wanazungumzia hilo kwa sababu bei za bidhaa na huduma zinaweza kuwa chini lakini hawana kipato cha kununua,” alisema Profesa Ngowi.
“Fedha imepungua kwenye mzunguko na wengi hawana ajira, hivyo ni lazima wataona ugumu wa maisha kwa sababu hata kama bei zitakuwa chini hawawezi kununua,” alisema Profesa Ngowi kwa njia ya simu jana.
Gavana Ndulu aliwaambia waandishi wa habari juzi kuwa fedha zipo na kwamba wanaolalamika kuwa zimepotea ni mafisadi ambao walikuwa wakizipata kwa njia zisizo halali, huku Rais Magufuli akisema kupotea huko kwa fedha kunatokana na watu kuzificha na akatishia kubadilisha noti.
Kiongozi wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe ndiye aliyefufua mjadala wa hali ngumu ya kiuchumi alipoliambia Bunge wakati akimuuliza swali Waziri Mkuu kuwa sekta ya uagizaji bidhaa, uuzaji nje, ujenzi na mzunguko wa fedha umeshuka, vitu vinavyoashiria kudorora kwa uchumi.
Katika utafiti huo uliofanyika kati ya Juni 4 hadi 20 mwaka huu, jambo la pili ambalo wananachi wana hamu ya kumuuliza Dk Magufuli ni masuala ya elimu ambayo yameshika asilimia tisa, afya (asilimia nane), miundombinu (asilimia sita) na maji (asilimia tano).
Hata hivyo, wananchi hao hawakuona umuhimu wa kuwauliza wabunge, madiwani na wenyeviti wao wa mitaa au vijiji suala hilo la gharama za maisha badala yake wengi wameguswa zaidi na matatizo ya barabara, maji, afya, elimu na utawala bora.
Katika maswali kwa mbunge na diwani, sehemu kubwa ya wananchi waliohojiwa walipenda kuuliza masuala ya barabara wakati kwa mwenyekiti wa kijiji wengi walipenda kuuliza masuala ya maji.
Utafiti huo wa Sauti za Wananchi uliofanyika kwa njia ya simu na kuhusisha wananchi 1,813 wa Tanzania Bara, unaeleza kuwa asilimia 96 ya wananchi waliohojiwa wamepongeza utendaji wa Rais Magufuli wakati watu saba kati ya 10 (asilimia 68) wakiridhika na utendaji wa wabunge.
Eyakuze alisema matokeo hayo yanasadifu utafiti wa Afrobarometer, ambao umekuwa ukionyesha marais wa Tanzania kuanzia wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa hukubalika kwa viwango sawa kabisa na viwango vya juu vya kukubalika vya marais wote wa Afrika.
“Hata hivyo, kiwango cha kukubalika cha Rais Magufuli katika utafiti mpya wa Sauti za Wananchi ni wa kiwango cha juu kuliko viwango vya kukubalika vya marais 128 wa Afrika uliofanywa na Afrobarometer,” alisema Eyakuze.
“Ni asilimia mbili ambao hawakubali Rais Magufuli labda wanaendelea kumpima utendaji wake.”
Mbali na kupima kiwango cha kukubalika kwa Rais, utafiti huo umepima umaarufu wa baadhi ya mikakati na hatua zilizochukuliwa na Dk Magufuli.
Matokeo ya utafiti huo unaoitwa ‘Rais wa Watu?’ unabainisha kuwa ufutaji wa watumishi hewa, usimamishwaji wa watumishi wabadhirifu ujulikanao kama utumbuaji majipu, elimu bure ni miongoni mwa masuala maarufu zaidi yanayofanywa na Dk Magufuli.
Wananchi saba kati ya 10 (asilimia 69) walivutiwa na hatua ya kuwaondoa watumishi hewa, asilimia 67 walifurahia elimu bure na wananchi sita kati ya 10 ya waliohojiwa walitaja kuwa uondoaji wa watumishi ni miongoni mwa mambo matatu bora kufanywa na Dk Magufuli.
Ziara za kushtukiza zilizokuwa zikifanywa na Rais mapema baada ya kuingia Ikulu Novemba mwaka jana na kuvutia wengi, zimeonekana kutokubalika baada ya wananchi watatu tu kati ya 10 kuvutiwa nazo. “Baadhi ya mikakati mikubwa ya Rais Magufuli imejitokeza chini kabisa kwenye orodha, likiwemo suala la ukwepaji wa kodi kwa kupata asilimia sita, kupambana na rushwa asilimia moja, kuzuia uagizaji wa sukari asilimia nne na kupunguza matumizi serikalini yasiyo ya lazima asilimia moja,” inasema ripoti hiyo.
Wananchi walipoulizwa ni vitendo gani vya Rais Magufuli ambavyo hawakubaliani navyo kabisa, watatu kati ya 10 (asilimia 32) walitaja suala la bei elekezi ya sukari, asilimia tisa walisema uondoaji wa watendaji wa umma na wananchi sita kati ya 10 (asilimia 58) walisema hakuna suala wasilokubaliana nalo.
Hata wakati kukiwa na mjadala mzito wa tuhuma za Serikali kuminya demokrasia baada ya Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya kisiasa kwa sababu za amani, ni asilimia sita tu ya waliohojiwa walisema hawakubaliana na Rais Magufuli katika “kuminya nafasi ya demokrasia.”
Licha ya wengi kuvutiwa na utumbuaji majipu, wananchi wanane kati ya 10 (asilimia 76) walitaka watendaji wa umma waondolewe iwapo tu kuna uthibitisho wa vitendo viovu.
Ni watu wawili tu kati ya 10 sawa na asilimia 24 waliosema mtendaji yeyote wa umma aondolewe mara moja pale anapohisiwa kufanya vitendo viovu.
Pamoja na wengine kuhitaji utawala wa sheria katika utumbuaji majipu, walioulizwa namna ya usimamishaji kazi watumishi hao, robo tatu ya waliohojiwa walisema “Rais awaondoe hadharani watumishi wa umma pale wanapotuhumiwa kufanya vitendo viovu”.
Hata hivyo, robo walisema wanakubali watumishi hao waondolewe lakini isifanyike hadharani.
Kuhusu madhara ya uondoaji watumishi hao, Eyakuze alisema wananchi tisa kati ya 10 wanasema kuwa kuwaondoa watendaji wa umma kutasaidia viongozi wengine kutozembea kazi.
“Wananchi hawa wanaamanisha kuwa kuwaondoa watendaji hadharani utakuwa mfano kwa wengine,” alisema Eyakuze.
Wachangiaji wengine walipongeza matokeo ya utafiti huo, lakini walikosoa kitendo cha Twaweza kuchelewa kutangaza matokeo kwa umma, hali ambayo inafanya utafiti huo usiakisi hali iliyopo sasa.
“Kama utafiti ulifanywa Juni mwaka huu kwanini hamkutoa (Twaweza) matokeo palepale ili tujadili?” alihoji mwandishi maarufu wa blogu ya Udadisi, Chambi Chachage wakati akitoa maoni yake kwenye uzinduzi huo.
“Hapa kati kuna mambo mengi yamepita kama la Chadema kutangaza operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta) na masuala ya kushuka kwa uchumi. Bila shaka matokeo ya sasa ya kukubalika kwa Rais yangekuwa tofauti.”
Mtafiti wa masuala ya uchumi, Dk Bohela Lunogela alisema utafiti unaweka misingi ya kufuatilia utendaji wa Rais Magufuli kwa kuwa umefanyika baada ya miezi na ukiendelea utaleta tija.
“Hii ya asilimia sita pekee kuonekana kuguswa na uminyaji wa demokrasia, sidhani kama ni sahihi. Kama utafiti ungefanywa hivi karibuni, matokeo yangekuwa tofauti,” alisema Profesa Mwesiga Baregu, mtaalamu wa masuala ya siasa na utawala.
Profesa huyo alisema amevutiwa na matokeo yanayoonyesha wananchi wengi kwa sasa wanataka utawala wa sheria kwa kutaka watumishi wa umma watumbuliwe baada ya kuthibitika kufanya maovu.
“Fungate limekwisha na sasa Watanzania wengi wameanza kuuliza haya matamko ya Rais yanayoonekana kwenda kinyume na Katiba. Wanataka kujua mipaka yake na ile ya kikatiba,” alisema.
Mhariri Mtendaji wa kampuni ya magazeti ya Serikali (TSN) Dk Jim Yonazi alipongeza matokeo hayo akisema kazi hiyo ya utafiti ilitakiwa ifanywe na vyombo vya habari, lakini bado ni jambo jema kufanywa na Twaweza.
Hata hivyo, alihoji namna ya uulizaji maswali hususan swali la “unamfahamu vipi kiongozi wako” ambalo alitaka limeng’enywe ili taarifa zitakazotoka ziwe na mashiko zaidi.


ConversionConversion