Samia awataka polisi wa SADC kudhibiti uhalifu


Makamu wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka Wakuu wa Majeshi ya Polisi Kusini mwa Bara la Afrika kuweka mipango na mikakati madhubuti ya kukabiliana na vitendo mbalimbali vya uhalifu vinavyotokea katika ukanda huo.

Amesema mipango hiyo itakuwa ni hatua ya kuhakikisha wananchi wanafanya kazi zao kwa amani na utulivu.

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo leo wakati anafungua mkutano wa Wakuu wa Majeshi ya Polisi Kusini mwa Afrika katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa AICC jijini Arusha, ambapo amesisitiza kuwa mkutano huo utakuwa ni chachu katika kuibua changamoto mbalimbali za kihalifu na kuzifanyia kazi ipasavyo kwa manufaa ya ukanda huo.

Amesema ni wajibu wa wakuu hao wa majeshi ya polisi ya kusini mwa Afrika kujiepusha na malalamiko yasiyo ya msingi kutoka kwa raia ambayo yanasababishwa na vitendo vya urasimu, uzembe na rushwa ili kujenga uwazi na uwajibikaji.

Makamu wa Rais pia amehimiza kudumishwa kwa ushirikiano miongoni mwa wakuu wa majeshi ya polisi kusini mwa Afrika katika kubadilishana mbinu bora za kukabiliana na vitendo vya uhalifu wa kuvuka mipaka.

Katika mkutano huo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini –IGP- Ernest Mangu amekabidhiwa uenyekiti wa Shirikisho la wakuu wa Majeshi ya Polisi kusini mwa Afrika (SARPCCO) kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Nchi ya Msumbiji Dos Santos JANE.

Shirikisho la SARPCCO lilianzishwa mwaka 1995 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa majeshi ya polisi kusini mwa Afrika katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika ukanda huo.
Previous
Next Post »