
Siku moja baada ya Rais John Magufuli kutoa muda wa siku saba kwa wizara na taasisi za Serikali zinazodaiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ziwe zimekamilisha malipo, joto limeanza kuonekana kwa baadhi yao kuanza kulipa na wengine kugoma kulizungumzia.
Juzi, Rais Magufuli alipokuwa akizungumza na wakazi wa Magomeni Kota jijini Dar es Salaam, alitoa agizo la siku saba kuhakikisha wadaiwa hao bila kujali taasisi au wizara waondolewe kwenye majengo hayo kwa nguvu.
Kabla ya agizo hilo, siku saba zilizopita NHC liliondoa vitu katika ofisi za gazeti la Tanzania Daima na ukumbi wa Bilicanas, mali ya mfanyabiashara, Freeman Mbowe anayedaiwa Sh1 bilioni na shirika hilo. Mbowe pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, alinukuliwa akisema pamoja na Bilicanas, shirika linazidai taasisi za umma, binafsi na watu binafsi jumla ya Sh15 bilioni.
Mchechu alitaja wadaiwa wengine kuwa ni Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi inayodaiwa Sh2 bilioni, Benki ya Azania Sh161 milioni, Wizara ya Mambo ya Nje Sh631 milioni, Wizara ya Afya Sh1.3bilioni, Tume ya Utumishi Sh109 milioni na Wizara ya Habari Sh1 bilioni.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana kuhusu kutakiwa kulipa madeni yao ndani ya siku saba, Profesa Faustin Kamuzora ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, alisema wizara yake imeshaanza kutekeleza agizo hilo, huku akiahidi kulipa ndani ya ukomo wa siku zilizotolewa.
Profesa Kamuzora alisema wizara hiyo imeshawasiliana na Wizara ya Fedha kwa ajili ya kuhakikisha inatekeleza agizo la Rais Magufuli.
“Huwezi kukwepa maagizo ya Rais kwa hivyo, tumeshaanza kutekeleza ila siwezi kukuambia ni kiwango gani tumeshalipa, baada ya siku mbili au tatu hivi unaweza kupata ‘feedback’ kwa NHC wanaohusika na ukusanyaji,”alisema.
Wakati Profesa Kamuzora akisema wizara yake inaendelea kulipa, Waziri wa Habari, Nape Nnauye alisema hajaona deni hilo kwenye wizara yake. “Wewe umeangalia ukaona wizara yangu imo? Sijaona hilo deni wala sijui,” alisema.
Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga alisema hana taarifa za kulipia deni la Sh631 milioni kwa NHC, kwa sababu wao walipangishwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
“Sisi tumepangishwa na ofisi ya AG na hatuna taarifa za kulipa deni kwa NHC,”alisema.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamisi Kigwangalla alisema hawadaiwi na NHC lakini anachokijua ni kwamba kulikuwa na mgogoro ambao NHC walikuwa wanadai eneo lililopo jengo la wizara hiyo ni lao.
“Mgogoro huo uliwahi kufikishwa mpaka kwa Rais aliyemaliza muda wake, lakini nashangaa NHC hawataki kukubaliana na maamuzi hayo,” alisema Dk Kigwangalla.


ConversionConversion