Kigoma kuwa mji mkuu wa mawese Afrika



Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma imesema inampango wa kuufanya mkoa wa Kigoma kuwa mji mkuu wa mawese barani Afrika ifikapo mwaka 2020.

Hayo yameelezwa na Meya wa Manispaa ya Kigoma-Ujiji Hussein Ruhava Juma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mpango wa Uwazi, Ushiriki na Uwajibikaji Serikalini (OGP) ambapo mji wa Kigoma umechaguliwa kushiriki katika mpango huo unaoshirikisha miji 15 duniani.

“Kama mjuavyo mawese ni zao kuu la biashara la wakulima mkoa wa Kigoma, kwa kipindi kirefu manufaa ya mawese hayajaonekana kwa uwazi kwa sababu ya kukosekana kwa soko la uhakika, uhaba wa viwanda vya kuongeza thamani pamoja na kutopandwa kwa miche mipya ya mawese, ” amesema.

Amesema manispaa ya Kigoma-Ujiji imepanga kupanda michikichi milioni 3 mji mzima kuanzia mwakani ili ifikapo 2020 mji huo uweze kuvuna mawese na mafuta ya kutosha katika kipindi cha miaka 25 mfululizo.

“Tunataka tuwe na uwezo wa kuvuna mawese na mafuta yenye thamani ya dola za kimarekani 83 sawa na sh. Bilioni 170 kwa mwaka,” alisema.

Aidha, amewataka wfanyabiashara wenye mitaji ya viwanda vya kuongeza thamani kuwekeza Kigoma kutokana kwamba inatarajia kuzalisha tani 80,000 za mawese ghafi kwa Mwaka kuanzia 2020.

Kuhusu mpango wa OGP, Meya Juma amesema manispaa yake imepata maendeleo kupitia mpango huo na kwamba kwa sasa wameweka vipaumbele 6 ambavyo vitatumika kama vigezo vya kupima utendaji kazi wa manispaa hiyo.

Ameitaja mipango hiyo kuwa ni sekta ya elimu, afya, maji, ardhi, uwazi katika bajeti na uwazi katika takwimu.
Previous
Next Post »