Waziri mkuu Kassimu Majaliwa amewahakikishia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera kuwa serikali iko makini katika kuratibu misaada inatolewa kwaajili yao na kwamba itawafikishia misaada waathirika wote bila ubaguzi.Waziri mkuu Kassimu Majaliwa ametoa kauli hiyo wakati akipokea msaada wa jumla ya sh. Bilioni 1.040 kutoka kwa watumishi na wadau mbalimbali zikiwa ni misaada kwa wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Septemba 10, mwaka huu ambapo amesema serikali itahakikisha misaada yote inavyotolewa inafika kwa walengwa.
Akikabidhi michango hiyo Balozi Kijazi amesema anaamini michango hiyo itasaidia kuwafuta machozi waathirika japo hakilingani na kile walichopoteza.
Waziri mkuu pia ametoa ufafanuzi juu ya malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya watu na waathirika wa tetemeko hilo kuwa misaada haiwafikii hali ambayo inawafanya waishi maisha magumu.
Katika hatua nyingine, waziri mkuu amepokea michango ya sh. Milioni 40 na kati ya hizo, sh. Milioni 20 zimetolewa na kampuni ya ujenzi ya CHICO ya China na sh. Milioni 20 nyingine zimetoka kwa umoja wa wafanyabiashara na wenye viwanda wa India waliopo nchini (India Business Forum).
Tetemeko hilo lililotokea Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu, lilisababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 kujeruhiwa huku nyumba 2,063 zikianguka na nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa.


ConversionConversion