Bukoba. Jengo la kihistoria la Kanisa Katoliki la Kashozi Jimbo la Bukoba ambalo mwili wa Kardinali wa kwanza Mwafrika Laurean Rugambwa ulilazwa kwa miaka 15 kabla ya kuzikwa rasmi limekimbiwa na waumini baada ya kuharibiwa na tetemeko la ardhi.Tetemeko hilo lililotokea wiki iliyopita limeharibu kanisa hilo na kuliacha na nyufa kubwa hali iliyowafanya waumini wa kanisa hilo kusalia nje.
Kabla ya kuanza kwa misa iliyoongozwa na Padre Francis Mutagwaba, waumini walitakiwa kuhamisha viti vilivyokuwa ndani ya kanisa hilo na kuviweka kwenye uwanja uliopo eneo hilo kwa ajili ya kuanza ibada.
Padre Mutagwaba alisema janga hilo limeathiri maisha ya wananchi wengi maskini na kutaka kundi hilo lisikandamizwe wakati wa taratibu za kupewa misaada alizosema tayari zimeanza kulalamikiwa kuwa na dosari.
Pia aliwataka watu wasitumie nafasi ya tetemeko la ardhi kujinufaisha badala yake waongeze nguvu katika kuwasaidia wananchi walioharibikiwa na makazi yao na kuhitaji msadaa wa chakula na faraja.
Paroko wa kanisa hilo, Padri Phillibert Mutalemwa alisema mpaka sasa hawajapata ufumbuzi wa kudumu wa sehemu watakayokuwa wanasalia kuwa mbali na kanisa, pia nyumba za watumishi ziliharibiwa.
Kanisa la Kashozi ambalo ndilo la kwanza katika Jimbo la Bukoba lilianza kujengwa mwaka 1892 na kufunguliwa mwaka 1904 ambapo mbali na vijiji mbalimbali jirani, pia linatumiwa na wanafunzi wa Sekondari ya wasichana Hekima na chuo cha Ualimu St Francis Nkindo


ConversionConversion