Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa ametangaza kumsimamisha kazi Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo Patricia Chisoti kutokana na uzembe uliosababisha kifo cha mtoto mchanga.
Akitangaza uamuzi huo, Madusa alisema amefikia hatua hiyo baada ya kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo kujiridhisha kuwa muuguzi huyo alipokuwa zamu alizembea kumuhudumia mama mjamzito na kusababisha kifo cha mtoto aliyekuwa tumboni.
“Mama huyo alikuja jana (juzi) ofisini kwangu na kunieleza hali hiyo, ndipo nilipoamua kukaa na kamati ya ulinzi na usalama pamoja na yeye, (Mariamu) na kumwita ambapo alituelezea hali ilivyokuwa kwa kweli ni kitendo cha uzembe ambacho hakitakiwi kufumbiwa macho,” alisema.
Awali Mkuu huyo wa wilaya na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Sophia Kumbuli wamejikuta wakiangua kilio mbele ya wagonjwa na wauguzi wa hospitali ya Wilaya hiyo baada ya Mwanamke mmoja kusimumulia namna alivyompoteza mtoto wake kutokana na uzembe wa Muuguzi wa zamu ambaye aligoma kumsaidia.
Viongozi hao walijikuta waliangua kilio baada ya Mwanamke huyo, Maria Mwaipasi kushindwa kujizuia na kuanza kutokwa na machozi wakati alipokuwa akiieleza kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya jinsi alivyompoteza mtoto wake wa kiume baada ya Muuguzi Mkunga aliyekuwa zamu Patricia Chisoti kukataa kumuhudumia.
Mwaipasi aliieleza kamati ya ulinzi na usalama kuwa alifikishwa hospitalini hapo na ndugu zake Septemba 4, mwaka huu majira ya usiku baada ya kuugua uchungu.
Alisema kuwa baada ya kufika hospitalini akiwa na wifi zake walibisha hodi kwenye chumba cha Muuguzi huyo ambapo hata hivyo hakuitikia kwa muda huo.
“Niligonga mlango muda mrefu bila kufunguliwa, ambapo baada ya muda mrefu huyo nesi alikuja na kumwambia wifi yangu anipe beseni alilokuwa amelibeba licha ya kuwa nilikuwa na hali mbaya kwa wakati huyo, mimi nikamwambia nesi siwezi kubeba akamuamuru wifi yangu anipe hilo beseni,” alisema.
Alisema baada ya kufika kwenye chumba kinachotumika kujifungulia ‘Leba’ akiwa hawezi hata kutembea alimwomba muuguzi huyo amsaidie ambapo alifika na kumkunja ukutani huku akimfokea kuwa anamsumbua kwani alikuwa amechoka usiku huo.
Mwaipasi alisema alipomweleza kuwa hawezi kutandika kitanda cha leba kutokana na hali yake muuguzi huyo alimfokea kwa kudai kuwa ile haikuwa kazi yake.
“Nilipotandika kile kitanda kwa shida sana nikawa nashindwa kupanda kitandani kutokana na uchungu wa kujifungua ndipo nikamwomba nesi tena lakini alinifokea kuwa namsumbua na haikuwa kazi yake huku akilalamikia kuwa mimi nina mdomo sana tangu nimefika hosptalini” alisema Maria.
Hata hivyo alisema alipokuwa kitandani mtoto alianza kutoka ambapo baada ya kumwita muuguzi na kumweleza alimjibu kuwa alikuwa bado hivyo alalie ubavu.
Alisema alivyokuwa amelalia ubavu huku akiendelea kumsukuma mtoto alimwita tena Patricia ambapo alimfokea kuwa anamsumbua kwani na yeye ni binadamu anahitaji kupata muda kwa kupumzika.
Alisema majira ya asubuhi alipelekwa kwenye chumba cha upasuaji na alitolewa mtoto wa kiume ambaye alikuwa tayari amepoteza maisha.
Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dr. Sasita Shabani alikiri kuwepo kwa matukio ya iana hiyo kwenye hopsitali hiyo na kuahidi kuyashughulikia mara moja.


ConversionConversion