Ndesamburo: Uteuzi wa JPM pasua kichwa


Moshi. Mwanasiasa mkongwe, Philemon Ndesamburo amedai hatua ya Rais John Magufuli kuteua wakurugenzi wa halmashauri nje ya mfumo wa Serikali, umewavunja moyo watumishi wengine.

Ndesamburo ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Moshi Mjini (2000-2015), alisema mfumo huo ulikuwa ukiwajenga watumishi kutoka madaraja ya chini hadi uandamizi, hao ndiyo walikuwa wakiteuliwa.

Julai 7, Rais Magufuli aliteua wakurugenzi 185 kati yao 65 ndiyo walioteuliwa kutoka orodha ya zamani ya wakurugenzi na 120 ni wapya.

Licha ya uteuzi huo, wapo wakurugenzi walioteuliwa ambao hawakuripoti vituo vya vya kazi na hivyo kumlazimu Rais Magufuli Septemba 10 kuteua wengine.

Kati ya hao wapya, wapo walioteuliwa miongoni mwa makada wa CCM walioshindwa kura za maoni ndani ya chama hicho 2015 na wengine wakitoka nje ya mfumo wa utumishi wa umma.

Ndesamburo alidai hatua ya Rais kuteua makada wa CCM nje ya mfumo kushika wadhifa huo, utaziyumbisha halmashauri nyingi kwani wengi hawajui namna ya kushughulikia madokezo.

“Kwenye baadhi ya halmashauri hao ambao walionekana hawawezi kuwa promoted (kuteuliwa), ndiyo wanaowafundisha wakurugenzi wapya. Hapa kidogo Rais wetu alichemka,” alidai Ndesamburo.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, Ndesamburo alidai nafasi za uteuzi kama za wakuu wa mikoa na wilaya, Rais angeweza kuteua makada wa CCM lakini siyo ukurugenzi.

“Huu utaratibu wake kwa kweli umewashangaza wengi na watumishi wengi wa halmashauri wanaumia lakini hawawezi kusema na kwa ukweli imewavunja moyo,” alisisitiza.

Ndesamburo anaungana na wanasiasa na wasomi waliokosoa uteuzi wa makada wa CCM, akiwamo kiongozi mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe aliyedai utaathiri uchaguzi 2020.

Previous
Next Post »