Marehem DK Didas Masaburi kuagwa Karimjee leo


MWILI wa Meya wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi, leo utaagwa na viongozi wa kitaifa pamoja wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kwenye Viwanja vya Karimjee, kabla ya kwenda kuzikwa katika Chuo cha ugavi na ununuzi cha IPS kilichoko Chanika wilaya ya Ilala.

Msemaji wa familia, Edson Fungo aliliambia gazeti hili jana kuwa, kwa kuwa Dk Masaburi alikuwa mwanasiasa na amewahi kushika nyadhifa mbalimbali kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikalini, familia imeona vyema watoe fursa ya kuagwa na wanasiasa wenzake pamoja na wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

Dk Masaburi kabla ya kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki. Wakati akiwa Meya alichaguliwa pia kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALART).

Hadi mauti yanamkuta, Dk Masaburi alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa Chuo cha IPS kilichoko Chanika nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Ni katika eneo la chuo hicho ndiko marehemu atazikwa leo. Ratiba iliyotolewa na Msemaji huyo wa familia hiyo, inaonesha kuwa saa 3.00 mwili ndio utawasili kwenye Ukumbi wa Karimjee na ibada itaanza saa 4.00 asubuhi.

Utasomwa wasifu wa marehemu na baadaye kutakuwa na neno kutoka kwenye Chama Cha Mapinduzi na viongozi wa serikali.

Shughuli ya kuaga mwili wa marehemu itaanza saa 5.00 na saa 6.30 mchana msafara kwenda Chanika utaanza. Utakapowasili kutafanyika ibada ya maziko na pia wananchi wa maeneo hayo na wanajumuiya ya IPS wataanza kuaga.

Jana ujenzi wa kaburi ambako atazikwa Dk Masaburi ulikuwa unaendelea katika eneo hilo la chuo na baadhi ya viongozi wa serikali na CCM waliwasili kwa ajili ya kuhani msiba huo.

Baadhi ya viongozi waliokuwepo jana ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bullembo na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhaga Mpina.

Dk Masaburi aliaga dunia usiku wa kuamkia Alhamisi wiki iliyopita katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alikuwa amelazwa akisumbuliwa na homa ya Ini (Hepatitis B).

Habari ya kifamilia inaeleza Dk Masaburi alikuwa akisumbuliwa na homa ya ini ambayo ilimsumbua kwa miezi kadhaa hadi mauti yanamkuta.

Ugonjwa huo ulimfanya aende India kutibiwa ambako alikaa kuanzia Februari hadi Agosti mwaka huu. Licha ya kurejea nchini, alikuwa na miadi ya kurudi tena India Novemba, mwaka huu kufanyiwa uchunguzi zaidi wa afya yake kujua anavyoendelea.

Lakini hali yake ilibadilika ghafla ndipo akapelekwa Hospitali binafsi ya Regency kupatiwa matibabu na alihamishiwa Muhimbili mwanzoni mwa mwezi huu.

Dk Masaburi ambaye kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita aliwania ubunge wa Ubungo kwa tiketi ya CCM na akashindwa, ameacha wake watatu, watoto 20 na wajukuu kadhaa.

Miongoni mwa wake zake na watoto wake pia ni wanasiasa.
Previous
Next Post »